skip to Main Content

MWANZA

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefanikiwa kukamata na kuteketeza shehena ya vipodozi na chakula zaidi ya tani tatu zenye viambata sumu na zilizoisha muda wa matumizi ambazo zilikamatwa kupitia ukaguzi maalumu uliofanyika katika maduka mbalimbali Kanda ya Ziwa.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuteketeza shehena hiyo lililofanyika katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza, Afisa udhibiti ubora TBS Kanda ya Ziwa Arnold Kubingwa amesema hatua hiyo inalenga kuondoa sokoni bidhaa zote zisizofaa kwa matumizi kwani zina madhara kwa watumiaji.

Kubingwa ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa wanazoziagiza na kuziuza zinakidhi matakwa ya viwango ikiwemo kuangalia tarehe ya uzalishaji na mwisho wa matumizi.

Naye Afisa usalama wa chakula TBS Kanda ya Ziwa, Elikaneny Minja amesema bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na ambazo zina viambata sumu ni hatari kwa afya ambapo zinaweza kusababisha maradhi ya ngozi ikiwemo kansa kwa watumiaji na kwamba madhara hayo yanaweza kuhamia kwa watoto walio tumboni ikiwa mtumiaji ni mjamzito.

Back To Top