skip to Main Content

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali waliojitokeza kumpokea katika uwanja wa ndege wa Mpanda.Picha na Samwel Mbugi

KATAVI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi(CCM) Dkt Samia Suluhu Hassan leo amewasili mkoani Katavi kwa ajili ya kufunga kilele cha wiki ya Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho Julai 13 na kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa huo.

Rais Samia amewasili katika uwanja wa ndege Mpanda na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja huo.

Aidha atakuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha wiki ya Jumuiya ya Wazazi kitaifa ambayo itafungwa Julai 13, 2024 katika uwanja wa CCM Azimio manispaa ya Mpanda.

Pia shughuli zitakazofanyika katika viwanja vya Azimio ni pamoja na kufanya ufungaji rasmi wa wiki ya wazazi pamoja na kufanya mkutano wa hadhara wa kiserikali kwa maana ya kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Katavi.

Mara baada ya kumaliza shughuli za uwanja wa Azimio Rais Samia atakagua eneo la ujenzi wa kituo cha kupozea umeme kilichopo Wilaya ya Mlele wa gridi ya Taifa unaotokea Tabora kuelekea mkoani Katavi.

Julai 14, 2024 Rais Samia atafungua jengo jipya la ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi na kufanya uzinduzi wa maghala ya kutunzia mazao mbalimbali katika eneo la Mpanda Hotel yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA), baada ya hapo atazindua bandari ya Karema.

Kadhalika, Julai 15, 2024 Rais Samia anatarajiwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi na kufanya mkutano wa ndani wa majumuisho na viongozi mbalimbali ndani ya mkoa kisha ataondoka kuelekea mkoani Rukwa na akiwa njiani kuelekea mkoa huo atasalimiana na wananchi wa Kata ya Kibaoni Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.

Kwa upande wao wananchi mkoani Katavi wamefurahishwa na ujio wa Rais Dkt Samia kwa kuwa hakuwahi fika mkoani humo tokea alipoteuliwa kuwa Rais.

Back To Top