skip to Main Content

HABARI 4.OCT,2021

KATAVI

Mufti Mkuu wa Tanzania,Sheikh Abubakar Zuberi kwa mara ya Kwanza anatarajiwa kufanya ziara Mkoani Katavi ambapo katika ziara yake atafungua na kuzindua Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Mkoa wa Katavi,kuzindua Ofisi za BAKWATA Mkoa pamoja na kuzindua Mpango mkakati wa maendeleo ya BAKWATA Mkoa wa Katavi wa Mwaka 2021/25.

Akizungumza Ofisini kwake Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Shekhe Mashaka Kakulukulu licha ya kuwahimiza Waumin kujitokeza katika Uwanja wa Ndege kumpokea Mfufti Siku ya Tarehe 5 Oktoba 2021 Asubuhi,amesema hadi sasa maandalizi yanaendelea vizuri na wamepokea Wageni kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa na Mikoa jirani wakiwemo Ma-sheikh.

Sheikh Kakulukulu ameongeza kuwa Mufti pamoja na Ujumbe wake watakagua pia Shamba la Mikorosho la Baraza Kuu la Waislam Katavi lililopo Kasekese ikiwemo kutoa Msaada wa Kibinaadamu kwa Watoto Yatima wapatao 100 kwa kutoa Sare za Shule.

INSERT..KAKULUKULU.

Aidha,amehimiza utulivu na mshikamano kipindi chote cha ugeni huo huku akisisitiza maandalizi yote ya kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19 yamezingatiwa kwa kuhakikisha Wataalam wa Afya wanapata wasaa wa kutoa Elimu Siku hiyo ikiwemo kutoa Chanjo kwa yule atakaye hitaji na amewataka Waumini na Wananchi kwa ujumla kuzingatia tahadhari zote.

Ziara hiyo ya Mufti Mkuu wa Tanzania,Sheikh Abubakar Zuberi ni sehemu ya Majukumu yake ya kutembelea Waislam Nchini.

TARIME. 

Watu wawili wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa baada ya magari mawili kugongana eneo la Gamasara wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/ Rorya,  William Mkonda amesema ajali hiyo imetokea jana  Oktoba 3, 2021  asubuhi.

Amesema ajali hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Zakaria na  gari aina ya Nissan Safari.

Kamanda Mkonda amesema chanzo cha ajali hiyo ni uendeshaji usiozingatia sheria za usalama barabarani hali iloyosababishwa na dereva wa basi.

Hata hivyo, amesema kuwa majina ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo bado hayajapatikana na kuahidi kutoa taarifa zaidi.

MOROGORO. 

Serikali imesema imekusanya kodi ya Sh1.9 trilioni kwa kipindi cha Septemba mwaka huu ikiwa ni sawa na asilimia 93.

Akizungumza na vyombo vya habari Oktoba 2, 2021 Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema makusanyo hayo ni makubwa kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2020.

Msigwa amesema serikali liweka malengo ya kukusanya Sh2.1trilioni, na kusema ukusanyaji huo ni mkubwa ukilinganisha na mwaka jana kipindi kama hiki ambapo walikusanya  Sh1.7 trilioni sawa na asilimia 80 ya malengo tuliyojiwekea ya kukusanya Sh2.2 trilioni.

DODOMA. 

Rais Samia Suluhu Hassan ameshangazwa na mmomonyoko wa maadili kwa vijana wakati kuna Chama cha Skauti Tanzania, Umoja wa Vijana wa CCM na wale wa vyama vya upinzani wanaotakiwa kuwahimiza vijana wenzao kuzingatia maadili.

Rais, ambaye ni mlezi wa Chama cha Skauti nchini, ameyasema hayo juzi, wakati wa hafla ya Siku ya Mlezi wa Skauti Tanzania ambayo haijafanyika tangu mwaka 1995.

Suala la mmomonyoko wa maadili limekuwa likishuhudiwa kutokana na tabia ya kuiga utamaduni wa magharibi.

Hata hivyo, Rais aliahidi kushirikiana na skauti kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwamo kuwafanya kuwa pamoja kati ya Skauti na Girl Guide.

Dodoma. 

Wakati hali za majeruhi wa ajali ya basi la Emigrace iliyotokea Juzi  wilayani Kondoa mkoani Dodoma , Jeshi la Polisi limesema linamshikilia dereva wa basi hilo aliyejisalimisha mwenyewe.

Mapema Oktoba 2, 2021 basi hilo linalofanya safari zake kati ya Babati Mkoa wa Manyara na Dar es Salaam lilipata ajali na kupinduka katika mtelemko wa milima ya Kolo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.

Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi amesema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na hadi sasa wamebaki 11 hospitalini.

Dk Ibenzi amesema majeruhi waliopelekwa hospitalini hapo walikuwa 15 lakini wanne wameaharuhusiwa baada ya hali zao kutengemaa kiasi.

Hata hivyo, amesema baadhi yao waliovunjika vioungo wanaendelea na matibabu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Onesmo Lyanga amesema wanamshikilia dereva wa gari hilo na kusema hadi sasa ajali hiyo imesababisha vifo vya watu tisa na maruhi kadhaa.

Kamanda Lyanga amesema kati ya vifo hivyo, watu wazima walikuwa sita na watoto wadogo walikuwa watatu.

KIMATAIFA

Vyama vya SPD na FDP vimekutana kwa mazungumzo ya kwanza mjini Berlin kujadili uwezekano wa kuunda serikali ya mseto.

Kabla ya hapo, chama cha SPD pia kilifanya mazungumzo na chama cha Kijani, Hali kadhalika muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU ulifanya mazungumzo na chama cha FDP.

Kimahesabu, kufuatia uchaguzi wa mwezi uliopita, kuna uwezekano wa kuundwa serikali inayoongozwa na SPD au muungano wa CDU/CSU.

Lakini kwa vyovyote vile, vyama vya FDP na Kijani vitahitajika kuunda serikali ya mseto.

OMAN.

Watu wapatao tisa wamekufa Oman na Iran hapo jana baada ya Kimbunga Shaheen kupiga katika maeneo ya pwani ya nchi hizo.

Nchini Oman maafisa wamesema watu wawili wamefariki kutokana na maporomoko ya ardhi na mtoto mmoja alifariki katika mafuriko.

Safari zote za ndege zimefutwa au kuahirishwa, kasi ya upepo ilipofikia kilomita 120 kwa saa moja kaskazini mwa pwani ya Oman.

Katika mji mkuu Muscat, maji yalijaa na kufunika matairi ya magari, hali iliyopelekea magari mengi kupungua barabarani.

Na kwa upande wa Iran, watu sita walikufa katika bandari ya Chabahar katika jimbo la kusini mashariki mwa Sistan-Baluchestan.

Shirika la habari la IRNA nchini Iran limesema miundombinu, vinu vya umeme na barabara, viliharibiwa na kimbunga Shaheen.

Back To Top